Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila imeadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kufanya mazungumzo na wagonjwa na ndugu wa wagonjwa kwa lengo la kupata maoni yao ili kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya hospitalini hapo.
Akiongoza zoezi hilo Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema hospitali imedhamiria kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wake hivyo maoni yao ni muhimu na yanamchango mkubwa katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Amesisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma, kununua vifaa tiba vya kisasa na kwamba jukumu lililopo ni kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi viwango na matarajio ya wateja.
“Tumekuja kuwasikiliza ili kupata maoni, ushauri na mapendekezo yenu ambayo kimsingi yatatusaidia katika utendaji ili kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma’’amesema Dkt. Magandi
Kwa upande wa baadhi ya wateja wametoa maoni na kupongeza wataalam kwa huduma nzuri wanazotoa na kueleza kuwa awali walisikia taarifa zisizo sahihi kuhusu MNH Mloganzila kwamba hakuna huduma bora lakini baada ya kufika hospitalini hapo wameshuhudia namna madaktari na wauguzi na wataalam wote kwa ujumla wanavyojituma na kufanya kazi zao kwa weledi.